Share news tips with us here at Hivisasa

Wizara ya ardhi na tume ya ardhi nchini NLC zimeanzisha mpango wa kuweka rekodi zote za maswala ya ardhi kwenye mfumo wa dijitali ili kuweza kuinua huduma zinazotolewa kote nchini.

Mfumo huo utapelekea Wakenya kupata huduma wanazozitaka na ambazo zinahusiana na ardhi kidijitali bila ya kutembelea afisi za wizara hiyo au tume husika.

Mpango huo utakaogharimu shilingi bilioni kumi aidha utapelekea kuwafukuza madalali laghai katika makao makuu ya wizara hiyo na ambao wamekuwa wakila pesa za Wakenya kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa NLC Mohammed Swazuri amesema kuwa ukosefu wa habari muhimu kuhusiana na ardhi kwa Wakenya umekuwa changamoto kubwa suala wanalotadhmini jinsi ya kukabiliana nalo.

Swazuri ameyasema haya Jumatano wakati wa kufunguliwa kwa warsha ya siku mbili kuhusu kuwekwa katika mfumo wa dijitali masuala ya ardhi katika hoteli moja mjini Naivasha.

“Tunaelewa masuala ya ardhi humu nchini ni nyeti na ndio maana tunataka kuondoa utata ambao umekuwa ukikumba wizara ya ardhi,” alisema Bw Swazuri.

Kwa upande wake Katibu wa kudumu katika wizara ya ardhi Mariamu El Maawy amesema kuwa huduma hii mpya itapelekea kurahisishwa kwa kupata habari kuhusiana na ardhi kwa Wakenya kwa haraka bila ya kupoteza muda mkubwa.

“Bila shaka itakuwa inarahisisha masuala tata ya ardhi,” alisema Bi Maawy.