Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung'aro amewakashifu wakosoaji wake na kuitetea hatua yake ya kuunga mkono mrengo wa Jubilee, licha ya kuwa alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM.

Akizungumza mjini Kilifi siku ya Jumatatu katika kampeni za kumpigia debe mgombea wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi, Mung'aro, alisema kuwa ODM walimtimua kama kiongozi wa wachache katika bunge la taifa, kwa madai kuwa yeye ni msaliti, hivyo hawezi waunga mkono tena.

Aidha, Mung'aro, amewataka wanasiasa wa Mombasa kukoma kujihusisha na siasa za Kilifi, na kudai kuwa walichangia kutimuliwa kwake ili mmoja wao ateuliwe.

“Wanasiasa wa Mombasa walikua katika mstari wa mbele kuhakikisha kua navuliwa wadhifa wangu. Nashangaa wamekuja Kilifi kufanya nini?” alisema Mung'aro.

Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alitetea chama cha ODM dhidi ya madai kuwa chama hicho hakijawafaidi Wakazi wa Pwani, licha ya kupigiwa kura kwa wingi katika uchaguzi uliopita.

Joho alisema kuwa ni vigumu kwa ODM kuzitekeleza baadhi ya ahadi zake kutokana na kuwa katika upande wa upinzani.

Hata hivyo, aliwahimiza wakaazi wa Kilifi kumpigia kura mgombeaji wa ODM katika uchaguzi huo.

Uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi umeratibiwa kufanyika Machi 7, na tayari Philip Charo wa Jubilee na Willy Mtengo wa ODM wanaonekana kuwa wapinzani wakuu, huku wadadisi wa kisiasa wakihoji kuwa huenda uchaguzi huo ukaashiria ubabe baina ya Cord na Jubilee.