Mwenyekiti wa Baraza La Magavana nchini Peter Munya ameikashifu vikali hatua ya idara ya usalama nchini kuwapokonya walinzi Magavana Ali Hassan Joho wa kaunti ya Mombasa na Amason Jeffason Kingi wa Kilifi.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa, Munya ambaye pia ndiye Gavana wa kaunti ya Meru ametaja hatua hiyo kama inayokandamiza demokrasia na ugatuzi katika serikali za majimbo.
Aidha Munya amemlaumu Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinet kwa kile amekitaja kama utumiaji vibaya wa mamlaka na uvunjanji wa sheria kwa kukosa kufuata taratibu zinazofaa kabla kuwaondoa walinzi hao.
Kauli ya Munya imeungwa mkono na naibu mwenyekiti Baraza La Magavana, Gavana wa kaunti ya Kilifi Salim Mvurya ambaye amedai kuwa hizo ni njama za serikali za kuwatishia viongozi wa upinzani baada ya kubwagwa katika uchaguzi mdogo wa Malindi.
Siku ya Alhamisi Gavana Ali Hassan Joho na Jeffa Kingi walipokonywa walinzi huku idara ya usalama ikisema kuwa maafisa hao wa polisi wanapelekwa kupata mafunzo zaidi.
Hata hivyo, Joho, siku ya Ijumaa katika mkutano na wakaazi wa Mombasa aliilaumu serikali akidai kuwa inamlenga kutokana na msimamo wake wa kisiasa.