Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa halmashauri ya kukabiliana na utumizi wa dawa za kulevya nchini Nacada, John Mututho, ameunga mkono pendekezo la kuvunjiliwa mbali kwa halmashauri hiyo kutokana na madai ya baadhi ya maafisa wake kujihusisha na ufisadi.

Akiongea siku ya Ijuma mjini Naivasha, Mututho alisema kuwa amekuwa katika mstari wa mbele kupigana na ufisadi katika shirika la Nacada na kusema kuwa iwapo kuvunjwa kwake kutasaidia kumaliza ufisadi, basi ataunga pendekezo hilo mkono.

Mututho alisema kuwa baadhi ya maafisa wa Nacada wamepora mailioni ya pesa kutoka shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika ya kijamii bandia.

Alidai kuwa baadhi ya maafisa hao walianzisha mashirika ya kijamii ili kunufaika kutokana na fedha zinazotolewa na Nacada kwa mashirika ya kijamii.

“Kuna watu ndani ya Nacada ambao wanataka kufilisisha shirika hilo na mimi kama mwenyekiti naunga mkono pendekezo la kuvunja shirika hilo ili liundwe upya baada ya kila afisa kufanyiwa uchunguzi wa mali yake,” alisema Mututho.

Aliongezea, “Hatuwezi kupigana na ufisadi ndani ya Nacada iwapo kuna watu fulani ambao wameandikisha mashirika bandia na wanatumia njia laghai kuyanufaisha na fedha za Nacada.”

Mapema wiki hii mwanachama wa bodi ya Nacada Charles Kanyi, al maarufu Jaguar, alitaka kuvunjiliwa mbali kwa shirika hilo kutokana na kile alichokitaja kama ufisadi uliokithiri ndani ya shirika hilo.

Tayari maafisa kumi na mmoja wa sharika hilo wanachunguzwa kutokana na madai ya kufuja pesa za shirika hilo.