Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa Wadi ya Changamwe Jimmy Ondari ameelezea masikitiko yake kutokana na hatua ya Kaunti ya Mombasa kupuuzilia mbali pendekezo la wawakilishi wadi la kutaka kubuniwa kwa kwa hazina ya maendeleo katika kila wadi.

Akizungumza siku ya Jumatano, Ondari alisema wanakumbana na wakati mgumu wa kuwaridhisha wakaazi licha ya kuwa wamekuwa wakiwahudumia ipasavyo, hali inayosababishwa na kutotengewa fedha zozote na serikali ya kaunti.

Haya yanajiri baada ya wakaazi wengi kusema kuwa hawana cha kujivunia kutoka kwa uongozi wa wawakilshi wa wadi, hasa katika upande wa miradi ya maendeleo.

Mwakilishi wadi huyo alisema kuwa hali hiyo imechangiwa na kutotengewa hazina yoyote mbali na hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge, almaarufu CDF.

Aidha, Ondari alisema kuwa hatua hiyo imezorotesha miradi mingi ya maendeleo kwenye wadi hasa ikizingatiwa kwamba mgao wanaopata kutoka kwa serikali ya kitaifa haiwezi kukidhi mahitaji yote ya wadi.