Mfanyikazi mmoja wa shule ya sekondari ya Moi mjini Nakuru anauguza majeraha baada ya kudungwa kisu na mwanafunzi.
Mfanyikazi huyo kwa jina maarufu J Muturi anasemekana kudungwa kisu Alhamisi wakati akitokea shuleni humo akiwa njiani kuelekea nyumbani.
Duru kutoka shuleni humo zinasema kuwa mwanafunzi aliyefanya uovu huo alikuwa wa kidato cha tatu na alikuwa amefukuzwa shuleni humo kwa muda baada ya nidhamu yake kuonekana mbaya.
Hata hivyo katika mahojiano na baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa wanadhania Bwana Muturi alidungwa kisu tokana na hatua yake ya kuwakazia wanafunzi.
Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo ya sekondari ya Moi Stephen Karanja alisema kuwa uchunguzi umeanzishwa.
Akizungumza shuleni humo Ijumaa asubuhi, Karanja amewataka wanafunzi kukumbatia mdahalo badala ya kuchukuwa sheria mikononi mwao.
"Najua kunaweza kuwa na matatizo ya hapa na pale lakini mdahalo ni muhimu katika kupata haki," alisema Karanja.