Mwanamke mmoja aliaga dunia huku mwanamume mmoja akiachwa na majeraha baada ya kuhusika katika ajali katika barabarani kuu ya Nyamira kuelekea Kebirigo
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Bondeni pale ambapo gari la kibinafsi lilikosa mwelekeo na kugonga mwendeshaji bodaboda aliyekuwa amebeba mwanamke huyo.
Akidhibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, afisa mkuu wa polisi wilayani Nyamira Rico Ngare, alisema kuwa marehemu Hellen Jurius, alifariki papo hapo baada ya kugongwa na gari hilo.
"Ajali hiyo iilitokea pale ambapo gari lilokuwa linatoka Nyamira kuelekea Kebirigo lilipoteza mwelekeo na kuwagonga mwendeshaji bodaboda na abiria wake. Abiria huyo alifariki papo hapo,” alisema Ngare.
Aliongeza, “Dereva wa gari hilo alitoweka na kuacha gari hilo hapa Bodendeni na kufikia sasa hajulikani aliko. Maafisa wangu wameanzisha uchunguzi na nina matumaini kuwa tutamkamata hivi karibuni.”
Mwendeshaji bodaboda huyo alipelekwa katika Hospitali ya Tenwek huku mwili wa marehemu ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nyamira.
Ngare amewaomba madereva kuwa makini wanapoendesha magari yao ili kulinda maisha ya watu.