Mwanamme mmoja wa umri wa makamo amepatikana amefariki mapema asubuhi ya Jumamosi katika kivuko cha ferry katika hali ya kutatanisha.
Walioshuhudia kisa hicho walisema mwanamme huyo alikuwa akifanya kazi ya kubebea wasafiri mizigo eneo hilo na alianza kutapika damu kabla ya kufariki.
Wakiongea na mwandishi huyu kwenye eneo la tukio, wafanyikazi wenzake walisema kuwa marehemu hakuwa na dalili za ugonjwa wowote na walishangazwa na kifo chake.
“Huyu jamaa huwa tunabebea watu mizigo na yeye hapa kila siku tukivusha upande wa pili wa Likoni na alikuwa mzima kabisa, sasa tunashangaa hatujui tatizo ni nini,” alisema mmoja wao.
Afisa mmoja wa Kenya Ferry wa kitengo cha usalama ambaye hakutaka jina lake kutajwa alimwambia mwandishi kwamba wanasubiri maafisa wa polisi kufanya uchunguzi kubaini chanzo chake.
“Hili ni jambo ambalo pia sisi limetushangaza na hatuwezi kusema lolote kwa sasa, tunasubiri polisi kuchukua mwili kisha watafanya uchunguzi zaidi,” aliongeza.