Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka sitini alipatikana akiwa ameuawa katika Soko la Nunga, kata ya Wamunyu, kaunti ndogo ya Mwala.
Akidhibitisha kisa hicho siku ya Jumapili, OCPD was Mwala Henry Rukaria, alisema kuwa uchunguzi umeanzishwa mara moja ili kubaini chanzo cha kifo cha mwanamume huyo.
Alisema kuwa mwili wa mwanamume huyo aliyekuwa mfanyakazi kwenye boma moja katika eneo hilo ulikuwa na majeraha ya panga.
"Hakuna mshukiwa ametiwa mbaroni kufikia sasa lakini uchunguzi umeanzishwa,” alisema Rukaria.
Aidha, Rukaria alisema kuwa polisi walimhoji mwajiri wa marehemu aliyewaelezea kuwa hajamwona mwanamume huyo tangu alipomwaga siku ya Ijumaa.
Vilevile, afisa huyo aliwataka wakaazi kushirikiana na polisi katika uchunguzi wa kifo hicho.