Serikali ya Kaunti ya Mombasa imekashifu hatua ya serikali kuu kuwataka maskwota wanaoishi katika Shamba la Waitiki kulipa pesa za kugharamia hati miliki katika ardhi hiyo yenye utata.
Serikali hiyo ilisema kuwa hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa serikali kuu haiko tayari kutatua mzozo huo, na kupata suluhu ya kudumu.
Hii inatokana na kizaazaa kilichoshuhudiwa katika ukumbi mmoja huko Likoni siku ya Jumanne, pale wakaazi walipotakiwa kulipa shilingi 182,000 pesa za kugharamia hati miliki.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba alisema kuwa wananchi wanaoishi katika shamba hilo ni maskini na hawawezi kulipa pesa hizo.
“Sisi kama kaunti tunafahamu kuwa maskwota wanaoishi katika shamba hilo wengi wao ni maskini na pesa hizo ni nyingi sana kwao kulipa. Tunaomba serikali kuu iwasaidie wananchi na sio kuwakandamiza,” alisema Njaramba.
Aidha, Njaramba alisema kuwa wanatilia shaka shughuli hiyo ya kutoa hati miliki huku akisema kuwa huenda zoezi hilo likakumbwa na mzozo zaidi kama ilivyoshuhudiwa katika maeneo mengine ya kaunti ya Mombasa.
“Tuliona mambo yalivyokuwa Mwakirunge na Ziwa la Ng’ombe, ambapo watu walipewa hati miliki na bado kukawa na mzozo zaidi. Hii yote ni kutokana na kufanya mambo bila kuwa na uwazi,” alisema Njaramba.
Kauli hii inakuja siku chache kabla Rais Uhuru Kenyatta ambaye yuko mjini Mombasa kwa sasa kutoa hati miliki kwa maskwota hao, zoezi linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi katika uwanja wa Caltex, Likoni.