Serikali ya kaunti ya Mombasa imeahidi kushirikiana na serikali kuu katika kutatua mizozo ya ardhi iliyopo katika kaunti hiyo.
Kaimu Waziri wa Ardhi, Makao na Mipangilio ya mji kaunti ya Mombasa Antony Njaramba amesema kuwa kaunti ya Mombasa ina zaidi ya shamba 71 ambazo hazipata hati miliki za ardhi kutokana na mizozo iliyopo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Njaramba amesema kuwa serikali ya kaunti ya Mombasa na serikali kuu zinaendeleza vikao vya mazungumzo kuhakikisha kuwa masuala ya uskwota kaunti ya Mombasa yanapata suluhu la kudumu kwa wakazi hao.
“Kama serikali ya kaunti ya Mombasa tuko tayari kushirikiana na serikali kuu kuhakikisha kuwa wakazi wetu wanapata suluhu la kudumu kuhusiana na suala la mzozo wa ardhi katika kaunti ya Mombasa,” alieleza Njaramba.
Amedai kuwa mazungumzo hayo yanatarajiwa kuwa na mwelekeo mwafaka ili zoezi la usorovea katika mashamba hayo kuanza kutekelezwa ili kuona kwamba mizozo ya ardhi inasitishwa katika kaunti hiyo.
Ardhi ya Nguu tatu huko Mwakirunge, Ziwa la Ng’ombe na donngo kundu ni kati ya ardhi zinazozozaniwa na lazima suala hilo kusuluhishwa.