Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema kuwa serikali yake imeweka mikakati kwa ushirikiano na washikadau wengine kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinaimarika.
Katika kikao na wakurugenzi mbalimbali wa Wizara ya Elimu ofisini mwake siku ya Ijumaa, Nyagarama alisema kuwa viwango vya elimu katika Kaunti ya Nyamira vinaendelea kudorora hata zaidi na kuwasihi wakurugenzi hao kushirikiana ili kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa.
Nyagarama alisema kuwa atafurahi sana ikiwa Kaunti ya Nyamira itakuwa miongoni mwa kaunti zitakazokuwa zimefanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa.
"Viwango vya elimu vimekuwa vikidorora huku Nyamira. Ni ombi langu kwenu wakurugenzi na washikadau husika kushirikiana kuhakikisha kuwa hali hiyo ya matokeo duni inarekebishwa. Kwa kweli itakuwa furaha yangu kama gavana kusikia kwamba Kaunti ya Nyamira ni miongoni mwa kaunti zitakazofanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa tunayo yatarajia," alisema Nyagarama.
Akizungumzia swala la ukeketaji wa wasichana Nyagarama alisema kuwa kamwe serikali yake kwa ushirikiano na ile ya kitaifa haitoruhusu tamaduni hiyo iliyopitwa na wakati kuendelea.
Alisema kuwa utamaduni huo ulikuwa ukichangia pakubwa katika kudhoofisha viwango vya elimu kwenye kaunti hiyo, huku akiwahimiza wakazi kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo badala yakujihusisha na tamaduni ziliyopitwa na wakati.
"Iwapo tunataka kuimarisha viwango vya elimu, sharti tuasi tamaduni za ukeketaji wa watoto wa kike kwa kuwa tamaduni hizo zinaathiri pakubwa elimu hasa ya mtoto msichana,” alisema Nyagarama.