Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema serikali yake imejitolea kuleta maendeleo zaidi kwa wakazi wa kaunti hiyo ili kutimiza ahadi alizotoa hapo mbeleni.

Akizungumza siku ya Jumatano mjini Nyamira, Gavana Nyagarama alisema serikali yake itahakikisha imefanya yale ambayo iliahidi kuyafanya haswa katika sekta ya afya na ukarabati wa barabara za kaunti, miongoni mwa miradi mingine.

“Naomba wananchi kuwa watulivu maana tunaendelea na kazi mliotuchagua kufanya. Nawahakikishia maendeleo zaidi katika kaunti yetu ili tuweze kusonga mbele kama jamii moja,” alisema Nyagarama.

Wakati huo huo, Nyagarama alisema ufisadi ni adui kwa maendeleo na kuna haja ya ufisadi kukomeshwa iwapo miradi ya maendeleo inatarajiwa kuafikiwa.

Aidha, alisema serikali yake imebuni kamati ya kuchunguza visa vyote vya ufisadi katika serikali ya Kaunti ya Nyamira.

“Tumebuni kamati itakayochunguza ufisadi miongoni mwa maafisa wa serikali na yeyote atakayehusishwa na visa vya ufisadi atakabiliwa kisheria,” alisema Nyagarama.