Huku usajili wa wapiga kura ukitarajiwa kufika kaditama mnamo siku ya Jumanne kote nchini, kaunti ya Nyamira imeonekana kuandikisha idadi ndogo ya wapiga kura mkoani Nyanza.
Akizungumza siku ya Jumapili katika wadi ya Gesima kaunti ya Nyamira kamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika wadi hiyo Pamela Otieno alisema kuwa kaunti ya Nyamira inavuta mkia kwa kuandikisha idadi ndogo ya wapiga kura.
"Katika kaunti ya Nyamira wale ambao wamejitokeza kujiandikisha hadi sasa ni wachache ikilinganishwa na kaunti zingine na idadi yao si ya kuridhisha,” alisema Otieno.
Wakati huo huo, Otieno aliomba wakaazi wa kaunti ya Nyamira kujitokeza kwa siku hizi mbili amabazo zimesalia ili kujiandikisha kama wapiga kura na kuwa na fursa ya kuwachagua viongozi wa watakao waletea maendeleo.
Aidha, chifu wa lokesheni ya Keroka Township Kennedy ndege naye alikashifu kitendo cha wakaazi kununuliwa na kujiandikisha katika sehemu zingine jambo ambalo halifurahishi hata kidogo.
"Naomba kila mtu kujiandikisha lakini si kununuliwa kujiandikisha kwingine na hiyo si furaha kwani viongozi wale mnahitaji hawatakuwa viongozi maana hamkuwapigia kura,” alisema Ndege.