Waziri wa Fedha na Ukusanyaji wa Mapato ya Kaunti katika kaunti ya Machakos alisema kuwa maandamano yaliyoendelezwa na wanabiashara mjini Machakos yalikua yamechochewa kisiasa, na maadui wa kisiasa wa serikali ya kaunti iliyo chini ya gavana Dr Alfred Mutua.
Bi Elizabeth Nzyoka alisema haya akihutubia waandishi wa habari katika ofisi yake iliyoko Machakos, siku ya Jumanne.
"Serikali ya kaunti ya Machakos haijaongeza ada zozote ili kuwadhulumu wanabiashara wetu kama walivyodanganywa na kufanywa waamini na wanasiasa wachochezi. Tulichokifanya ni kusawazisha kodi ili kuhakikisha usawa kwenye biashara zote katika ukusanyaji ya mapato ya serikali yetu ya kaunti," alieleza Waziri Elizabeth.
Aidha, wanabiashara hao walidai kuwa serikali hio ya kaunti ya Machakos iliongeza kodi kwa asilimia mia tatu, na kuwa hawakuhusishwa kwenye mswaada wa kifedha wa mwaka wa 2015. Mwenyekiti wa 'Chamber of Commerce' mjini Machakos, Bwana Simon Kitheka amewataka wanabiashara kutolipa kodi izo mpya na kudai kuwa watapeleka kesi hiyo kotini.