Share news tips with us here at Hivisasa

Kamanda wa polisi eneo la Mombasa Martin Asin ameaga dunia katika ajali ya barabarani kwenye eneo la Maungu, katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumannne, mshirikishi wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa alisema kuwa afisa huyo wa polisi alikuwa peke yake katika gari lake la kibinafsi alipogongana ana kwa ana na trela.

Marehemu aliaga dunia alipokuwa akipelekwa Nairobi kupokea matibabu.

Asin hapo awali alihuduma katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi kama naibu OCPD, na mwezi Agosti akapelekwa Mombasa kama OCPD.

Katika rambi rambi zake, Marwa alimtaja marehemu kama afisa mchapa kazi huku akitoa wito wa utulivu kwa wananchi serikali inapopanga mazishi yake.

Wakaazi wa Mombasa, eneo la Kisiwani, sasa wanataka dereva aliyehusika katika ajali hiyo kuchuliwa hatua za kisheria.

Wakiongozwa na Abdul Khatib, wakaazi wa Kizingo walisema kuwa itakuwa bora iwapo dereva huyo atakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ukiukaji wa kanuni za barabara.

Aidha, amewataka madereva kuwa waangalifu wakiwa barabarani ili kupunguza visa vya ajali.