Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kuajiri wahudumu zaidi wa afya katika Hospitali ya Gucha iliyoko eneo bunge la Bomachoge, ili kuimarisha huduma za afya katika hospitali hiyo.
Akizungumza siku ya Jumatano alipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Gucha, Ongwae alisema serikali yake itaongeza wahudumu wa afya katika hospitali hiyo ili kuimarisha huduma za afya.
Ongwae aliahidi kuboresha Hospitali ya Gucha ili wagonjwa waweze kupokea huduma bora.
Alisema kuwa hatua hiyo pia itapunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii.
“Serikali yangu imejitolea kuimarisha sekta ya afya. Nitaajiri wahudumu zaidi wa afya na pia nitaweka mashine za kisasa ili kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali ya Gucha,” alisema Ongwae.
Wakati huo huo, Ongwae alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo ili kuona jinsi maendeleo hayo yamefanywa na kuahidi kufanya mengine zaidi.
Miongoni mwa miradi ya maendeleo ambayo gavana huyo alitembelea ni miradi ya kuwekwa taa wilayani Gucha na eneo la Ogembo, ukarabati kwa vyoo katika soko la Ogembo, ukarabati wa maktaba ya vitabu na miradi ya maji miongoni mwa miradi mingine.