Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kushirikiana na shirika la Kenya National Highways Authority (KeNHA) kukarabati na kuziba mashimo katika barabara inayotoka Daraja moja kuelekea mjini Kisii.

Hii ni baada ya gari aina ya Nissan iliyokuwa inatoka eneo la Keroka siku ya Jumanne, kuhusika kwenye ajali katika eneo hilo, huku watu watano wakipoteza maisha yao.

Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii alipofika katika eneo hilo la ajali, Ongwae alisema serikali yake itashirikiana na KeNHA kuhakikisha mashimo yote katika barabara hiyo yamezibwa ili kupunguza visa vya ajali barabarani.

“Barabara hii ni mbovu zaidi kwani ina mashimo mengi ambayo yanastahili kuzibwa. Serikali yangu itajaribu kila iwezalo kwa ushirikiano wa KeNHA kukarabati barabara hii,” alisema Ongwae

Wakati huo huo, Ongwae aliahidi kukarabati barabara zilizoko chini ya uongozi wa kaunti, na kuomba serikali ya kitaifa kuhakikisha barabara zilizoko katika hali mbaya zinashughulikiwa inavyostahili kwa kukarabatiwa.

Aidha, Ongwae aliomba madereva kujali maisha ya binadamu na kuwaonya dhidi ya kuendesha magari kiholela, kwa kusema kuwa gharama ya maisha ya binadamu haijulikani.