Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idara ya usalama katika eneo la Pwani imesema kuwa imepokea ripoti za kijasusi kuwa kuna kiongozi mmoja wa kisiasa katika Kaunti ya Mombasa anayefadhili makundi ya kihalifu ya 'Wakali Kwanza' na 'Wakali Wao'.

Kwenye mahojiano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Juamatatu, Mshirikishi mkuu wa utawala katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa alisema kuwa anachunguza mienendo ya kiongozi huyo wa kisiasa pamoja na mawasiliono anayofanya na makundi hayo ya kihalifu, na lazima atakabiliwa.

Marwa alisema kuwa maafisa wa kijasusi wamebaini kuwa njama kuu ya kiongozi huyo ni kuvuruga usalama wa Kaunti ya Mombasa pamoja na kuzua taharuki miongoni mwa wakaazi wa kaunti hiyo.

"Tumepata ripoti za kijasusi kuwa mheshimiwa mmoja ambaye ni mbunge anafadhili makundi ya kihalifu ili kuzua vurugu katika Kaunti ya Mombasa. Nawahakikishia kuwa hili halitawezekana hapa Mombasa na kwengine kote kule katika ukanda huu wa Pwani. Serikali iko macho na inawafatilia kwa karibu viongozi kama huyo na lazima watakamatwa,” alisema Marwa.

Marwa alisema kuwa kila Mkenya ana haki ya kuishi popote katika taifa hili na lazima viongozi wanaopanga njama ya kuzua vurugu kutiwa mbaroni.