Maafisa wa polisi katika Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na idara ya usalama katika Kaunti ya Lamu wanamsaka mshukiwa wa uhalifu al maarufu Mungiki.
Mshukiwa huyo anadaiwa kuhusika katika visa tofauti vya uhalifu katika Kaunti ya Mombasa na kujificha Lamu.
Akizungumza siku ya Jumatatu kwenye kikao na wanahabari, Kamanda wa polisi katika eneo la Pwani Francis Wanjohi, alisema kuwa jamaa huyo ana uhusiano wa karibu na kundi la uhalifu lililoko Lamu linalofahamika kama Mbwamjumali.
Wanjohi alisema kuwa wamefanikiwa kumnasa mshukiwa mwengine wa uhalifu anaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja ya kibinafsi Mombasa, ambapo wanasubiri apate afueni ili waweze kumfungulia mashtaka.
Kwa upande wake, kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kuwa mlanguzi mmoja wa mihadarati amejisalimisha kwa idara ya usalama.
Haya yanajiri huku Halmshauri ya Bandari nchini KPA ikitoa ufadhili wa shehena moja itakayotumika kama kituo cha polisi kwenye ufuo wa bahari ya Jomo Kenyatta.