Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josephine Onunga ameagiza maafisa wa polisi kuwapiga risasi wezi wa ng’ombe mpakani Borabu-Sotik pindi wanapofumaniwa ili kupunguza visa vya wizi katika maeneo hayo.

Agizo hilo limetolewa baada ya visa vya wizi wa ng’ombe kuendelea kuongezeka mpakani Borabu-Sotik, jambo ambalo limepelekea jamii ya Kisii kupata hasara kubwa.

Akizungumza siku ya Jumapili katika kikao cha baraza kilichoandaliwa katika eneo la Borabu, Onunga alisema wao kama polisi hawatavumilia kuona wizi ukiendelea kukithiri, na kusema mshukiwa yeyote wa wizi wa ng’ombe akifumaniwa atapigwa risasi na kuuawa papo hapo.

“Naagiza maafisa wa polisi kufyatulia risasi wale ambao watafumaniwa wakitekeleza wizi katika eneo hili la Borabu-Sotik,” alisema Onunga.

Aliongeza, “Tumekuwa tukitoa onyo ili watu wajiepushe na vitendo vya wizi lakini jinsi inaonekana hawataki kututii. Sasa mkono wa serikali utawakabili vilivyo.”

Aidha, Onunga alisema kuwa wizi umekuwa ukigawanya jamii za Kisii na Kipsigis, lakini sasa ana imani kuwa utata huo utasuluhishwa kwa vile mshukiwa wa wizi akifumaniwa hatapata amani kamwe.

Matamshi hayo yaliungwa mkono na wakazi wa eneo hilo ambao walipokea agizo hilo kwa furaha.

Onunga aliomba wananchi kutoa ripoti kwa vituo vya polisi kuhusu mshukiwa yeyote wa wizi wa ng’ombe ili waweze kukabiliwa kisheria.