Maafisa wa polisi katika kitengo cha ujasusi, Kaunti ya Nyamira wameanza kuwachunguza washukiwa wawili wa duka la jumla la shiffling lililoko mjini Nyamira kwa madai ya kutekeleza wizi katika duka hilo.
Duka hilo lilivunjwa lango la nyuma na washukiwa siku ya Jumapili usiku huku wakifanikiwa kuiba pesa kiwango kisichojulikana .
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nyamira siku ya Jumatatu mkuu wa polisi katika kaunti ya Nyamira Karimbo Mwandoe alisema maafisa wa polisi wa kitengo cha ujasusi wameanza kuwachunguza walinzi wawili wa duka hilo kubaini jinsi wizi huo ulivyotekelezwa.
Hata hivyo mkuu huyo wa polisi alisema wanaendelea na uchunguzi wao huku wakitumia camera za siri maarufu CCTV zilizokuwa kwa duka hilo ili kujua waliotekeleza wizi huo.
“Walinzi wawili waliokuwa wakilinda siku hiyo wanaendelea kuchunguzwa ili kubaini jinsi wizi huo ulitekelezwa,” alisema Karimbo Mwandoe mkuu wa polisi nyamira.
“Kiwango cha pesa kilichoibiwa hadi sasa hakichabainika lakini baada ya uchungunzi tutapata mwelekeo mwafaka,” aliongeza Mwandoe.
Mwandoe aliwaonya wanaoendelea kufanya wizi akisema siku zao zinaendelea kuhesabiwa na watakapotiwa mbaroni watakabiliwa kisheria.