Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa mtaa wa Maweni eneo bunge la Nyali, Kaunti ya Mombasa, wameitaka idara ya usalama kushika doria kikamilifu ili kuzuia kukithiri kwa visa vya kihalifu.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, wakazi hao walisema kuwa kumechipuka makundi ya kihalifu yanayosababisha hofu ya kiusalama miongoni mwao.

Walisisitiza kuwa lazima usalama uimarishwe kufuatia kuchomwa kwa mshukiwa wa wizi na wahudumu wa bodaboda usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi.

Wakazi hao sasa wanahofu kuwa huenda kukazuka uhasama baina ya mitaa jirani kwani wanaotekeleza visa hivyo vya kuwachoma wezi ni wahudumu wa bodaboda na wanafaa kuripoti wahalifu kwa maafisa wa polisi.

“Tayari tumeingiwa na hofu ya kuzuka uhasama baina yetu na mitaa jirani kufuatia kuchomwa kwa mshukiwa wa wizi. Mtaa huyo hauna njama yoyote ya kuwahukumu vijana na tunaomba wahudumu wa bodaboda kuwaripoti wahalifu kwa maafisa wa polisi wala sio kuchukua hatua mikononi mwao,” alisema Salma Mwenye, mkazi.

Akithibitisha kisa hicho Naibu Chifu wa eneo hilo Bernard Omollo alisema kuwa usalama wa eneo hilo unafaa kuimarishwa huku akilaani tukio hilo lililotekekezwa na wahudumu wa badobado, akisema kuwa wakazi hawafai kuchukua hatua mikononi mwao bali kuwahusisha maafisa wa polisi.

“Tunashtumu kitendo cha vijana hao wa bodaboda kwa kutekeleza jukumu la kihalifu. Kama serikali hatutakubali hilo na tutaishikiza serikali kutuma maafisa wake wa polisi kuimarisha usalama,” alisema Omollo.