Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa eneo la Kisauni mjini Mombasa wamewataka maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wanayakabili magenge ya kihalifu katika eneo la Kisauni ili kuimarisha usalama wa eneo hilo.

Wakaazi hao wakiongozwa na mzee wa mtaa wa eneo hilo Khamis Abdallah walisema kuwa kuna haja ya maafisa wa polisi kutumwa katika eneo hilo kuhakikisha kuwa usalama wa eneo hilo unaimarishwa.

Akizungumza katika baraza la jamii katika eneo hilo siku ya Alhamisi, Abdallah alisema kuwa wazee wa mtaa katika eneo la Kisauni wataungana na kuwashauri vijana kujitenga na magenge ya kihalifu kama njia moja ya kudumisha amani.

“Kama wazee wa mtaa wa eneo hili, tumekubaliana kuungana na kuishinikiza idara ya usalama kutuma maafisa wake katika eneo hili kukabiliana na magenge ya kihalifu, ili eneo hili kuwa salama. Tutawashauri vijana wa eneo hili kuhakikisha kuwa wanadumisha amani,” alisema Abdallah.

Eneo la Kisauni linakabiliwa na changamoto ya kiusalama, kufuatia kuibuka kwa magenge ya kihalifu kama vile Wakali Kwanza na Wakali Wao.