Maafisa wa polisi mjini Nakuru Jumatatu waliwanasa washukiwa wanne wanaodaiwa kuchochea uvamizi wa makundi mawili mwishoni mwa wiki jana katika eneo la Flamingo viungani mwa mji wa Nakuru yaliyopelekea afisa mmoja wa polisi kujeruhiwa.
Wakiongozwa na afisaa mkuu wa polisi wa utawala Barnabas Kimutai maafisa hao pia waliweza kunasa pombe haramu lita 120 na dawa za kulevya aina ya bhangi wakati wa msako huo.
Kimutai amesema kuwa kadi za simu kadhaa pia zilipatikana na wahalifu hao.
"Tumewanasa watu hao baada ya kufanya uchunguzi wa kina na hivi karibuni tutawafungulia mashtaka," alithibitisha Bw Kimutai.
Aidha wanne hao wanadaiwa kuwa kundi la watu ambao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi na kuwapora hela zao kwa njia za ulaghai.
Aidha inadaiwa kuwa maafisa wa polisi wanaendeleza uchunguzi ili kuwanasa washukiwa wengine waliosalia huku wakiwataka wananchi kujitokeza na kutoa ushahidi katika lengo la kusitisha uovu huo mjini.
Ni wiki jana ambapo vijana wawili waliokuwa wakielekea nyumbani majira ya jioni walivamiwa na kujeruhiwa na kundi moja linalojitambulisha kama Confirmed kisa kilichozua taharuki katika eneo hilo na hata maeneo jirani na kupelekea kundi lingine linalojitambua kama Dragon kutaka kulipiza kisasi.
Hata hivyo hali hiyo iliweza kuthibitiwa na maafisa wa polisi mjini Nakuru walioshuhudiwa wakishika doria mchana na usiku kucha.