Vijana Mombasa wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuangazia maswala yanayowakumba anapoendelea na ziara yake katika eneo la Pwani.
Akizungumza siku ya Ijumaa mjini Mombasa, Kiongozi wa vijana katika mji huo Omar Kea alisema kuwa vijana wengi wamejitosa kwenye utumizi wa dawa za kulevya na makundi haramu kama vile kundi la 'Mombasa Republican Council' (MRC) kutokana na ukosefu wa ajira.
Kea aliwahimiza viongozi kutoka Kaunti ya Mombasa, na kaunti zote katika ukanda wa Pwani kwa jumla, kuhakikisha kuwa kongamano la vijana limeandaliwa.
Alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha vijana kuwasilisha matakwa yao kwa viongozi mbalimbali, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta.
Garama Kasiwa, kijana kutoka Mombasa, ameitaka serikali kuendeleza na kukuza talanta miongoni mwa vijana, kama njia moja ya kukabiliana na utumizi wa mihadarati katika jamii.