Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Rais Uhuru Kenyatta amewataka wananchi kukoma kuikosoa serikali mara kwa mara kuhusu uwepo wa jeshi la KDF nchini Somalia na badala yake kuwapa wanajeshi hao nafasi kuyatekeleza majukumu yao.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari katika Ikulu ya Rais mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Rais Kenyatta amesema lazima kila Mkenya afahamu kuwa taifa linahitaji usalama na umoja ili kufanikisha maendeleo na ukuaji wa uchumi.

"Usalama wa taifa hautambui ukabila, dini, msimamo wa kisiasa ila umoja na utengamano. Ni jukumu letu kama serikali kumhakikishia kila mwananchi usalama wake," alisema Rais.

Aidha, amesema kuwa jeshi la KDF kwa sasa linaendelea na shughuli ya kuwasafirisha humu nchini wanajeshi waliojeruhiwa katika shambulizi lililotekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab siku ya Ijumaa iliyopita katika eneo la El-Adde.

Kwa mjibu wa idara ya usalama, tayari majeruhi 20 pamoja na miili minne ya wanajeshi walioangamia katika shambulizi hilo imekwisha safarishwa nchini.

Rais Kenyatta vilevile, amesema kuwa idara ya jeshi itahakikisha kuwa wanajeshi waliowawa katika shambulizi hilo, wanazikwa kulingana na sheria na kanuni za jeshi.

Kwa upande wake Waziri wa Usalama wa nchi Raychelle Omamo, amewaahidi familia za waadhiriwa kuwa watakua wa kwanza kupokezwa taarifa kuhusu jamaa yao.

Kauli ya Rais hata hivyo inajiri wakati baadhi ya viongozi mbalimbali nchini, wakiwemo wakijamii na wakisiasa wakizidi kuihimiza serikali kuwaondoa wanajeshi hao nchini Somalia.

Siku ya Jumatau shirika la kutetea haki za binadamu la Muhuri, lilihimiza serikali kuliondoa jeshi la KDF nchini Somalia, huku akisema hatua hiyo itasaidia kulitokomeza shambuli la kila mara linalotekelezwa na Al Shabaab.