Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa tume ya kuwaajiri walimu TSC tawi la Mombasa, Ibrahim Rugut, amezitaka vyama vya kutetea haki za walimu Knut na Kuppet, kukoma kuwapotosha walimu kuhusu kandarasi ya utendakazi.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa baada ya kukamilika kwa kongamano lililowaleta pamoja walimu mjini humo, Rugut alizikashifu Knut na Kuppet, kwa kile alichokitaja kama kuwashawishi baadhi ya walimu nchini kususia kutia saini kandarasi hiyo kama walivyoagizwa na TSC.

Kulingana na Rugut, kandarasi hiyo itawawezesha walimu kupandishwa ngazi kulingana na utendakazi na juhudi zao, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo mwalimu angepandishwa cheo bila kutathmini mchango wake darasani, ila kwa kuzingatia muda aliohudumu.

“Knut na Kuppet zinawapotosha walimu. Kandarasi ya utendakazi itaiwezesha TSC kujua ni mwalimu yupi anajituma darasani ili mwalimu kama huyo apandishwe cheo kulingana na juhudi zake,” alisema Rugut.

Rugut vilevile alithibitisha kuwa zaidi ya walimu 150 wanaohudumu katika Kaunti ya Mombasa, tayari wametia saini mkataba wa utendakazi na TSC.