Wadau katika sekta ya utalii katika eneo la Pwani, hususan Kaunti ya Mombasa, wamedhihirisha matumani yao ya kuimarika kwa sekta hiyo msimu huu wa likizo.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Chama cha Wamiliki na Wahudumu wa Mahoteli kanda ya Pwani Sam Ikwaye, kuwasili kwa meli za watalii zaidi ya nne katika kipindi cha miezi miwili kumesaidia pakubwa kushamiri kwa sekta hiyo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa afisini mwake, Ikwaye alisema kwamba hatua ya serikali ya mataifa ya Uingereze, Marekani, Australia na Ufaransa kuondoa marufuku ya raia wao kutozuru pwani imechangia pakubwa kufufua sekta hiyo.
Ikwaye amewataka viongozi wa serikali pamoja na wale wa upinzani kushirikiana kwa karibu mno katika kupiga vita ugaidi, na kutafuta suluhu la kudumu ili sekta ya utalii kuzidi kuimarika baada ya kukumbwa na changamoto nyingi kwa muda mrefu.
“Kama chama cha wamiliki na wahudumu wa mahoteli, tunafuraha kuona kwa wageni na watalii wameanza kuzuru eneo la Pwani. Hiyo ni ishara kamili kuwa sekta ya utalii imeanza kurejea kama kawadi na tunamatumani msimu huu tutafaulu zaidi,” alisema Ikweye.
Ikwaye alisema sharti Wizara ya Usalama wa ndani pamoja an vitengo vyote vya kiusalama kushirikiana kubuni njia mbadala za kuzuia ugaidi na kukabiliana na washukiwa wa ugaidi, ili kuhakisha usalama unaimarishwa na kumudu sekta ya utalii nchini.