Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o amewasuta walioibua madai kuwa anashiriana kisiri na serikali ya Jubilee.
Akihutubu katika eneo la Bondeni, kwenye hafla ya kuchangisha pesa siku ya Jumapili, Seneta Okong’o alisema kuwa uungaji mkono wake kwa muungano wa Cord ni dhabiti.
"Wacha niwadhibitishie kuwa mimi ni mwanachama wa Cord na uungaji mkono wangu kwa muungano huo ni dhabiti. Madai kuwa ninashirikiana kisiri na Jubilee ni ya uongo,” alisema Okong’o.
Akizungumzia suala la madai kuibuliwa na baadhi ya magazeti humu nchini kuwa anatofautiana na Seneta wa Mombasa Hassan Omar Okong’o alisema kuwa madai hayo ni ya uongo na akawarai Wakenya kuyapuzilia mbali.
"Nimekuwa nikafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana na Seneta Omar hata kabla ya kuwa seneta kwa kuwa mimi pia ni wakili wa kutetea haki za kibinadamu. Madai hayo yanayoibuliwa na baadhi ya magazeti ni ya uongo," alisema Okong’o.
Okong’o alisema kuwa kamwe hawezi fanya kazi na muungano wa Jubilee kwa kudai kuwa muungano huo umeshindwa kukabili ufisadi ambao unazidi kukithiri kwenye idara mbalimbali serikalini.