Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kaunti ya Nyamira amesema licha ya rasimu ya katiba kupitishwa miaka mitano iliyopita, ufisadi ungali unakithiri miongoni mwa idara mbalimbali serikalini.

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira Senata Kennedy Okong'o alisema jinamizi la ufisadi linaweza tu kukabiliwa iwapo Rais Uhuru Kenyatta atajitolea kuhakikisha ufisadi unakabiliwa vikali serikali.

"Ufisadi ni janga kubwa ambalo taifa hili linakumbana nalo. Kwa kweli, ufisadi unaweza tu kukabiliwa iwapo Rais Kenyatta atajitolea kuhakikisha kuwa maafisa wanaohusishwa na ufisadi wamekabiliwa kisheria," alisema Okong'o.

Okong'o vilevile aliisuta tume yakukabili ufisadi nchini EACC kwa kutohakikisha maafisa wanaohusishwa na visa vya ufisadi wamechukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, alisema kuwa tume hiyo haifai kumtisha kiongozi wa muungano wa Cord Raila Odinga kwa kuwa anayosema ni kweli.

"Kazi ya Tume ya EACC ni kubweka tu bila makali ya kuuma kwa maana kuna kesi nyingi tume hiyo inazopokea bila kuchukua hatua za kisheria. Tume hiyo pia haistahili kumtisha kiongozi wa muungano wa Cord kwa kuwa eti yuaibua maswala ya muhimu na yaliyo na uzito," alisema Okong'o.