Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong'o ameahidi kushirikiana na Gavana John Nyagarama kufanya kazi kwa minajili ya kustawisha kaunti hiyo kimaendeleo.

Akizungumza kwenye hafla yakupokeza shule mbalimbali vitabu vya kusoma kwenye Shule ya msingi ya Nyamira siku ya Jumanne, Seneta Okong'o alisema kuwa kwa muda uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao, viongozi wanastahili kushirikiana kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo imekamilishwa.

"Kwa kweli huu ndio wakati wa kwanza naungana kufanya hafla ya pamoja na Gavana Nyagarama na nipo tayari kushirikiana naye ili kustawisha maendeleo kwenye kaunti hii, kwasababu tumesalia na muda mchache sana kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema Okong'o.

Okong'o aidha alimwomba Gavana Nyagarama kuwahusisha viongozi wengine wa kisiasa hasa anapofanya maamuzi muhimu kwenye serikali yake akiongezea kuwa wanacho hitaji wananchi ni ushirikiano wa maendeleo na wala sio malumbano.

"Nataka kumpa Gavana Nyagarama changamoto kushirikiana nasi anapofanya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuwa nasi pia ni viongozi waliochaguliwa kuwakilisha wananchi kwenye nyadhifa mbalimbali. Wananchi wanataka kuona tukishirikiana kufanya miradi ya maendeleo na wala sio kulumbana, " alisema Okong'o.