Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kununulia hospitali katika eneo bunge la Bomachoge Chache dawa za kutosha ili kuimarisha sekta ya afya katika eneo hilo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya hospitali katika eneo bunge hilo hazina dawa za kutosha.
Wakizungumza siku ya Jumapili katika eneo la Sengera, katika mkutano wa vijana wa eneo bunge la Bomachoge Chache, vijana hao wakiongozwa na mwenyekiti wa vijana katika eneo bunge hilo Dennis Kamau, walisema hospitali za eneo bunge hilo hazina dawa za kutosha.
Kamau alisema kuwa wakaazi hulazimika kutafuta matibabu katika hospitali za mbali.
Wakaazi hao waliiomba serikali ya kaunti kuhakikisha suala hilo limeshughulikiwa kikamilifu.
Baadhi ya hospitali ambazo zilitajwa kuwa na uhaba wa dawa ni Omorembe, Sengera na Mochorwa.
“Wakazi wa eneo hili hutembea masafa marefu wakitafuta matibabu wanapougua. Wao hulazimika kuenda mapka mjini Kisii maana zahanati na hospitali za eneo hili hazina dawa za kutosha,”alisema Kamau.
Aliongeza, “Tunaomba serikali ya kaunti kutukumbuka maana hatuwezi piga kura tukiwa wagonjwa. Lazima kwanza tiba ipatikane kwa hospitali zetu.”
Aidha, Benson Osoti, kijana, alidai kuwa serikali ya kaunti imekuwa ikitenga eneo hilo katika miradi ya maendeleo hasa, ukarabati wa barabara.