Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Kisii imetakiwa kuwajibikia majukumu yake na kuhakikisha kuwa mrundo wa takataka ulioko mjini Kisii umeondolewa.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa mjini Kisii, baadhi ya madereva, wafanyibiashara na abiria katika kituo cha magari mjini Kisii walisema kuwa waliopewa jukumu la kuzoa taka katika mji huo wanapaswa kuwajibika na kuondoa uchafu huo kwani unaendelea kuathiri mazingira.

“Hii si mara ya kwanza kwa mrundo wa taka kuachwa kukaa katika eneo hili kwa muda mrefu. Tunaomba wanaofanya kazi hii ya usafi mjini Kisii kuondoa uchafu huu kwani uko na harufu mbaya sana,” alisema Jackson Morara, dereva.

Wakaazi hao walisema kuwa sheria za mazingira nchini haziruhusu uchafu kuachwa kutapakaa jinsi inavyoshuhudiwa mjini Kisii, na kutaka suala hilo kushughulikiwa kwa haraka.

“Tunaomba wanaosimamia masuala ya mazingira katika Kaunti ya Kisii watusaidie kutatua changamoto hizi ambazo zinaendelea kutukumba. Huenda tukaathirika na maradhi mbalimbali yanoyasababishwa na mazingira machafu,” alisema Lydiah Nyasimi, mfanyibiashara.

Abiria nao walikashifu waliotwikwa jukumu la kuzoa taka katika eneo hilo kwa kutofanya kazi walioajiriwa kuifanya.