Kutokana na mzozo wa mpaka unaoendelea katika soko la Keroka baina ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii, sasa serikali za kaunti hizo mbili zimepanga kukutana siku ya Jumatano kutafuta suluhu.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumatatu, gavana wa kaunti hiyo alisema ni jambo la kushangaza kuona jamii ya Abagusii ikizozana katika swala ambalo linaweza kusababisha umwagikaji damu.
"Ni jambo la kushangaza kuona kuwa watu wanapigania mpaka kule Keroka hali ambayo yaweza sababisha umwagikaji damu na ndio maana sharti sisi kama viongozi tuketi kutafuta mwafaka wa suala hili mara moja," Nyagarama alisema.
Kwa upande wake mwakilishi wa wadi ya Rigoma, iliyoko katika eneo hilo lenye mzozo, Benson Sironga amesema iwapo lolote halitaafikiwa kwenye mkutano huo wa viongozi siku ya jumatano wataitisha ushauri wa mamlaka ya mpito kuhusu ugatuzi kutoa suluhu.
"Sehemu inayoibua mzozo kule Keroka inajulikana wazi kwamba ipo kwenye himaya ya serikali ya kaunti ya Nyamira,” Sironga alisema.