Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali imetakiwa kuzingita haki za kibinadamu kwa mujibu wa katiba ya nchi ili kuona kwamba unyanyasaji na dhulma za kijinsia zinasitishwa.

Mkurungezi mkuu wa shirika la utetezi wa haki za kibinadamu Muhuri, Hassan Abdille amesema kwamba idadi kubwa ya viongozi wa serikali pamoja na maafisa wa umma wamekuwa katika mstari wa mbele kuwakandamiza wananchi, hali ambayo imechangia taifa hili kukumbwa na changamoto nyingi.

Katika mkutano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu Abdille alisema kwamba wangehakikisha wamejitolea kikamilifu kupigania haki za Wakenya ili kuhakikisha kuwa dhulma hizo zimepungua kwa kiwango kikubwa.

“Tumeona kuwa baadhi ya viongozi wa serikali na maafisa wa umma wanatumia mamlaka yao vibaya na kuwanyanyasa Wakenya mali yao haswa wengi wakifurushwa katika ardhi zao huku wengine wakidhulumiwa kijinsia. Hatua hiyo kamwe sio demokrasia tuliyoipigania,” alisema Abdille.

Wakati huo huo ameshtumu kuongezeka kwa mauaji ya kiholela yanayokisiwa kutekelezwa na baadhi ya maafisa wa polisi kwa tuhuma za kukabiliana na magaidi nchini, akisema kwamba hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa serikali inakiuka haki za kibinadamu.

“Tunasikitishwa na jinsi maafisa wetu wa polisi wanavyotekeleza mauaji ya kiholela wakisingizia kukabilina na magaidi ilhali wanaua watu wasio kuwa na hatia, sisi kama shirika tunaishtumu hatua hiyo vikali,” aliongeza Abdille.