Mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo ya Kibiashara ya Rift Valley iliyoko Mjini Nakuru, John Gitau amezitaka serikali za kaunti na ile ya kitaifa kutenga kiwango fulani cha pesa kwa taasisi mbalimbali humu nchini.
Akizungumza katika sherehe ya kufuzu kwa mahafala wa taasisi hiyo katika Shule ya Upili ya Menengai, mkurugenzi huyo alisema taasisi mbalimbali hapa nchini zimekuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana.
Gitau alisema kwamba pasi na kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya kibiashara, hatma ya taifa hili kukua kimaendeleo bado ni ya kutiliwa shaka.
Aidha, mkurugenzi huyo alisema kuwa itachukua muda mrefu ili kumaliza umaskini nchini, iwapo vijana hawatawezeshwa.
“Vita dhidi ya pombe haramu na matumizi ya mihadarati ambavyo vinaendelezwa na serikali hapa nchini, huenda visifaulu ikiwa vijana hawatawezeshwa kikamilifu,” alisema Gitau.
Gitau alipendekeza viongozi kutoka nyanja mbalimbali kushikana mikono kwa pamoja kwa ajili ya kuwawezesha vijana ipaswavyo humu nchini.