Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa walimu wa shule za msingi za umma KEPSHA katika Kaunti ya Mombasa umeitaka serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza ahadi iliyotoa kwa wasimamizi wa shule hizo ya kupeleka pesa za elimu ya bure.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa Muungano huo katika kaunti ya Mombasa Fuad Ali alisema kuwa hadi kufikia sasa shule hizo bado hazijapokea pesa zozote kutoka kwa serikali, hali aliyoitaja kuwa imechangia changamoto kwenye uratibu wa mipango ya maendeleo katika shule hizo.

Ali alisema kuwa licha ya kuiarifu Wizara ya Elimu kuhusu tatizo hilo, bado halijashughulikiwa na kuitaka serikali kulishughulikia suala hilo.

“Tunashangazwa na serikali hadi kufikia sasa bado haijatuma pesa kwa shule na kutusababishia changamoto nyingi katika mipangilio ya shule. Licha ya Wizara ya Elimu kufahamu hili, bado suala hili halijatekelezwa,” alisema Ali.

Kauli ya Mwenyekiti huyo wa KEPSHA katika Kaunti ya Mombasa imejiri huku walimu wakuu wakizidi kukosolewa kwa kuongeza ada ya malipo ya karo kwa madai kuwa serikali imeshindwa kuiwajibikia suala la elimu ya bure.