Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa bucha mjini Kisii Joseph Maiko, ameiomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuunganisha umeme katika kichinjio cha Daraja Mbili ili kuimarisha shughuli za biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika eneo la Daraja Mbili, Maiko alisema kuwa serikali ya kaunti ilikuwa imeaahidi kuunganisha umeme katika kichinjio hicho lakini bado haijatimiza ahadi hiyo.

Maiko alisema kuwa kichinjio hicho husabambaza nyama katika bucha zilizoko mjini Kisii, lakini ukosefu wa nguvu za umeme umezuia biashara hiyo kunoga zaidi.

Mwenyekiti huyo alisema wanastahili kuendeleza shughuli zao hata nyakati za usiku au mapema asubuhi, lakini hawawezi kutimiza hayo kufuatia ukosefu wa umeme.

“Serikali ya kaunti ilituahidi kuwa itaunganisha umeme katika kichinjio hiki lakini inaonekana ni kana kwamba walisahau ahadi hiyo. Naomba serikali ya kaunti kutimiza ahadi ilizotupa na kutuunganishia umeme,” alisema Maiko.

Aidha, mwenyekiti huyo aliiomba serikali ya kaunti kuwakarabatia kichinjio hicho.