Huku zikisalia siku mbili kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa hati miliki kwa wakaazi wanaoishi katika Shamba la Waitiki, serikali ya kaunti ya Mombasa imetaka maskwota katika maeneo ya Mwakirunge na Ziwa la ng’ombe kupewa hati miliki pia.
Kaimu mkuu wa Idara ya Ardhi, Makao na Mpangilio wa Mji Antony Njaramba alisema kuwa serikali inafaa kuwaangazia wakaazi wa maeneo hayo kwani wanapitia changamoto zinazostahili kusitishwa na serikali kuu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Junatano, Njaramba alisema kuwa matokeo ya hivi majuzi ya wakaazi wa eneo la Nguu Tatu huko Mwakirunge, Ziwa la ng’ombe na Kalahari eneo la Changamwe kufurushwa katika ardhi zao na mabwenyenye, yanahitaji kusitishwa ili wakaazi hao kutekeleza miradi katika ardhi zao.
Alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na wadau mbalimbali watahakikisha kuwa migogoro ya ardhi katika kaunti hiyo inapata suhulu la kudumu.
"Sisi kama serikali ya Kaunti ya Mombasa tutahakikisha kuwa serikali imetoa hati miliki za ardhi kwa wakaazi wa Kaunti ya Mombasa wala sio tu wakaazi wa Shamba la Waitiki pekee,” alisema Njaramba.
Njaramba aliahidi kuishinikiza serikali kuhakikisha linashughulikia maeneo ya makaazi ya Kaunti ya Mombasa ambayo hayana hati miliki.