Mashirika ya kijamii katika eneo la Pwani yameitaka idara ya usalama kuhakikisha kuwa imeweka usalama wa kutosha katika eneo bunge la Malindi na hususan ukanda wa Pwani hata baada ya kukamilika kwa uchaguzi mdogo wa Malindi.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Mkurugenzi wa Shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre, Phyllis Muema amesema kuwa hatua inayoendelea kwa sasa katika eneo bunge la Malindi kuhusiana na uchaguzi wa eneo hilo unafaa kutizamwa kwa makini na maafisa zaidi wa usalama kuwekwa katika eneo hilo.
Muema alisema kuwa kushuhudiwa kwa msukosuko wa kuwahaonga wapiga kura huenda ukasababisha uhasama zaidi, na kusababisha eneo hilo kuwa na vurugu.
Alisema kuwa ipo haja ya maafisa wa usalama zaidi kutumwa katika eneo hilo na kanda nzima ya Pwani.
“Tunaitaka serikali kutuma maafisa zaidi wa usalama katika eneo la Malindi na pia Pwani kwa jumla kwa sababu msukosuko unaoshuhudiwa kwa sasa Malindi wa wakaazi kuvurugana na baadhi ya viongozi kwa sababu ya kuwahonga ili wawachague wafuasi wao huenda ukaleta uhasama zaidi,” alisema Muema.
Wakati huo huo, amewataka wakaazi wa eneo la Malindi kuwa watulivu na kusubiri matokeo ya uchaguzi huo mdogo na kuyakubali yatakapotanguzwa na Tume ya IEBC.