Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu katika bunge la Kaunti ya Nakuru Emma Mbugua amehimiza serikali kujenga shule zaidi za watoto wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo.

Mbugua alisema kuwa hatua hiyo itapelekea watoto wanaosihi na ulemavu kupata nafasi nzuri zaidi ya kupata elimu, huku akiashiria kuwa shule zilizotengewa walemavu katika Kaunti ya Nakuru ni chache mno ikilinganishwa na idadi ya walio na ulemavu kwenye kaunti hiyo.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Jumatano, Bi Mbugua alisema kuwa baadhi ya shule zilizotengewa walio na ulemavu katika Kaunti ya Nakuru zinakumbwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa madarasa ya kutosha.

Aliitaka serikali kulishughulikia swala hilo kwa kupanua shule zilizopo na pia kwa kujenga madarasa zaidi na vyoo kwenye shule hizo.

Alitoa mfano wa shule ya msingi ya Menengai ambayo alisema haina madarasa na vyoo vya kutosha.

Aidha, pia alitoa mfano wa shule ya upili ya Ngala aliyosema kuwa inafaa kuongezwa madarasa pamoja na uwanja wa shule hiyo kupanuliwa.

Alisema kuwa hatua hiyo itasadia kuhakikisha kuna uwepo wa mazingira mwafaka kwa wanafunzi.