Wafanyikazi wa kiwanda cha nguo cha EPZ katika eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa, sasa wamewataka viongozi wa kaunti hiyo kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wanarejeshwa kazini mara moja.
Wafanyikazi hao wanawalaumu viongozi hao kwa kunyamza kimya licha ya masaibu wanayopitia tangu kiwanda hicho kilipowasimamisha kazi mapema mwaka huu.
Wafanyikazi hao walikuwa wakizungumza siku ya Alhamisi wakati walipofanya maandamano ya amani katikati mwa jiji hilo kabla kuelekea katika afisi ya mshirikishi wa usalama katika ukanda wa Pwani.
Akiongea na wanahabari katika uwanja wa Makadara Grounds, mwakilishi wa muungano wa wafanyikazi hao Bi Mueni Kilonzo aliomba serikali kuu kutafuta suluhu ya matatizo yao.
“Tumemlilia gavana wetu lakini hatuoni mabadiliko yoyote na sasa tunamuomba rais aingilie kati kwa sababu tunaona kama kaunti imeshindwa,” alisema Bi Mueni.
Wafanyikazi hao zaidi ya elfu mbili walisimamishwa kazi baada ya kiwanda hicho kusema kuwa hakuna pesa zaidi za kuendelea kuwalipa kutokana na mauzo kurudi chini.
Hata hivyo, wafanyikazi hao walipinga madai hayo kwa kusema kuwa hiyo ni njama tu ya kuwanyanyasa kwani bidhaa zimekuwa zikinunuliwa licha ya kiwanda hicho kudai mauzo kupungua.
“Kila siku tulikuwa tukiona bidhaa tunazotengeza zikiuzwa na tunaposikia mauzo yameshuka, tunashidwa kuamini,” alisema mfanyikazi mmoja.
Wafanyikazi hao sasa wanashinikiza kiwanda hicho kuwarejesha kazini kwani wanadai tangu kusimamishwa kazi, imekuwa vigumu kumudu mahitaji yao ya kifamilia.
Siku ya Jumanne wakuu wa kiwanda hicho walifanya kikao na kamati ya leba ya bunge la Mombasa ambapo kamati hiyo iliitaka kampuni kufuata taratibu za kisheria na kuwarejesha kazini wafanyikazi hao.