Share news tips with us here at Hivisasa

Huenda shughuli za masomo katika shule za msingi zikasambaratika iwapo fedha zinazonuiwa kugharamia elimu ya msingi ya bure zitacheleweshwa.

Akizungumza huko Changamwe siku ya Ijumaa, Katibu wa Chama cha Walimu Knut katika Kaunti ya Mombasa Dan Aloo alisema kwamba kucheleweshwa kwa fedha hizo kumetatiza mno shughuli za masomo.

Aloo alisema kuwa ni sharti Waziri wa Elimu Fred Matiangi kuhakikisha kwamba fedha hizo zinawasilishwa shuleni kwa muda unaofaa.

Aidha, Aloo ameitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba nyongeza ya mishahara ya walimu ya asilimia 50-60 inalipwa kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Februari, ili kuwawezesha walimu kutekeleza majukumu yao shuleni kikamilifu badala ya kupitia hali ngumu ya kimaisha.

Aloo alisema kwamba walimu waliipigania nyongeza hiyo kihalali na ni lazima wapewe haki yao badala ya serikali kuendelea kuwakandamiza.

“Nitawashawishi walimu wenzangu kusitisha shughuli zao za kuwasomesha wanafunzi iwapo nyongeza hiyo haitatimizwa,” alisema Aloo.

Katibu huyo alisema kuwa amesikitishwa na jinsi serikali inavyoidunisha sekta hiyo ya elimu, na kusema kwamba ni sharti serikali kupitia Wizara yaelimu iwajibikie vilivyo sekta ya elimu nchini, kwa kuwatimizia walimu matakwa yao.

Kumekuwa na vuta ni kuvute kati ya walimu na serikali tangu mwaka jana, hali iliyopelekea Waziri wa Elimu wa hapo awali Jacob Kaimenyi kuhamishwa Wizara ya Ardhi huku mwezake wa mawasiliano Fred Matiangi akipewa jukumu hilo la kuidhibiti sekta ya elimu nchini.