Shirika la MUHURI, ambalo ni la kutetea haki za waislamu pamoja na watu ambao hawana uwezo wa kujimudu kusimamia kesi katika mahakama, limesema kuwa litajitahidi zaidi kuendelea kuwatetea wanyonge katika jamii hata kama wana changamoto za fedha.
Shirika hilo limesema kuwa bado lina uwezo wa kuwasimamia wakazi kutoka maeneo mbalimbali kutoka Kaunti sita za Pwani, ingawa akaunti zao zilifungwa na serikali bado wana ari na moyo wa kushirikiana na maafisa wa polisi pamoja na idara ya mahakama kuona kuwa haki ya watoto na kina mama na wanyonge inashughulikiwa katika njia ya sawa bila mapendeleo.
Akiongea siku ya Jumanne katika afisi yake, afisa anayesimamia kitengo cha watoto na jinsia ya kike kwenye shirika hilo la Bi Topster Juma alisema kuwa sharti mashirika ya kijamii kukaza misuli na kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuwapa uhai wa matumaini wale ambao wako katika hali ngumu ya kujikimu katika kujitetea kwenye mahakama za Kenya, huku akisema kuwa inakuwa vigumu kwa wengi wa waathiriwa kupata haki bila kuwa na hela ya kuwa na wakili mahakamani.
Juma alitoa wito kwa wakazi wa maeneo ya Pwani kutafuta msaada wa kisheria kutoka kwa shirika hilo ambalo mbali na kuwawakilisha watu kortini pia linajihusisha katika utoaji wa ushauri wa sheria na jinsi ya kukabiliana na baadhi ya kesi zinazowahisisha wateja wao.
Afisa huyo alisisitiza kuwa huduma zao huwa wanazitoa bure, na hawatozi ada yoyote ili kupewa ushauri wa kisheria na wana afisi kila eneo kwenye Kaunti za Pwani.