Share news tips with us here at Hivisasa

Mayatima na watoto walio na matatizo katika jamii kutoka wadi ya Ekerenyo, kaunti ya Nyamira wamepata sababu ya kutabasamu, baada ya shirika moja la kijerumani kuwapa ufadhili wa kifedha. 

Akihutubu wakati wa kutembelea vituo mbalimbali vya watoto mayatima siku ya Ijumaa, mwakilishi wa shirika la Alpha International tawi la Kenya Jackline Dency aisema kuwa waliteua wadi ya Ekeronyo baada ya kupata udadisi kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nyamira kuwa eneo hilo lilikuwa na idadi kubwa ya watoto mayatima wasio na msaada. 

"Tunataka kufuata utaratibu ili kuhakikisha kuwa tunawapa mayatima usaidizi wa kifedha ili waweze kupata masomo ndio waweze kujitegemea siku za mbeleni," alisema Dency. 

Afisa huyo aliongeza kusema kuwa shirika hilo limewasaidia mayatima kwa zaidi ya kaunti kumi na sita, huku akiongeza kusema kuwa anatumai shirika hilo litaendelea kuwasaidia mayatima zaidi. 

"Kufikia sasa tumeweza kuwapa usaidizi mayatima kwenye kaunti kumi na sita na tunatarajia kuwa tutaendelea na juhudi za kuwasaidia mayatima zaidi," aliongezea Dency. 

Kwa upande wake afisa msajili kwenye Wilaya ya Nyamira kaskazini Davis Okemwa alilihimiza shirika hilo kuendelea na mradi huo wa kuwasaidia mayatima, huku akiongezea kusema kuwa viwango vya juu vya mayatima vinaipa changamoto serikali ya kaunti ya Nyamira. 

"Ningependa kuhimiza shirika hili kuendelea kuwasaidia mayatima katika kaunti hii kwa kuwa idadi yao nyingi inaipa changamoto serikali ya kaunti kuafikia matakwa yao," alisema Okemwa.