Shuguli za kawaida katika afisi za serikali ya kaunti ya Nakuru mjini Naivasha zilitatizika pakubwa mapema Jumatatu baada ya usambazaji wa stima kukatizwa na shirika la Kenya Power.
Tukio hilo limeacha afisi nyingi ikiwemo ile inayotumiwa na Gavana Kinuthia Mbugua kila mara anapozuru mji huo bila stima huku ikiibuka kuwa wana deni la maelfu ya pesa.
Kufuatia hatua hiyo, wakazi wengi waliokuwa wamefika eneo hilo kutafuta huduma maalum wamebidika kurudi nyumbani huku maafisa wakuu wa serikali hiyo wakifanya mkutano na Kenya Power ili kujaribu kurejesha hali ya kawaida.
Mfanyikazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema kuwa usambazaji huo umekatizwa kwa sababu wakuu wao walikuwa wamekosa kulipa ada hizo ambazo zimeongezeka maradufu.
“Ni deni ya kampuni ya Kenya Power ndio imekuwa kubwa na kupelekea kukatwa kwa huduma za umeme, wanaoongoza hapa wamekuwa wakiletewa bili lakini hakuna anayeshughulika kulipa,” alisema mfanyikazi huyo.
Mkuu msimamizi wa serikali hiyo mjini Naivasha Julius Nyaata amedhibitisha hali hiyo na kusema kuwa tayari swala hilo limeangaziwa.
Nao Wawakilishi wa wadi (MCA,s) Simon Wanango na Esther Njeri wameitaka serikali hiyo kuharakisha kulipa deni hilo ili shughuli za kawaida zirejee.