Shule ya upili ya St John's Karunga eneo la Bahati, imepata ufadhili wa shilingi milioni moja kukamilisha ujenzi wa madarasa yanayoweza pia kutumiwa kama ukumbi wa mikutano kutoka kwa hazina ya ustawishaji eneo bunge la Bahati, CDF.
Kando na kitita hicho cha pesa, wanafunzi 57 kutoka shule hiyo aidha walipata basari ya shilingi 197,000.
Wanafunzi hao ni wale wanaotoka katika familia maskini, kulingana na mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri.
Kwa jumla, hazina ya CDF imetoa hundi za takriban shilingi milioni 1.49 kupitia basari katika muda wa wiki mbili, kusaidia wanafunzi wanaohitaji karo katika eneo bunge la Bahati.
“CDF ambayo mimi ni kinara wake, na Antony Njui ni mwenyekiti, itahakikisha kwamba tunapea kipau mbele maswala ya elimu ya watoto wote bila ubaguzi” Ngunjiri alisema.