Shule mbalimbali za umma kutoka kaunti ndogo ya Borabu zimelaumiwa kutokana na matokeo duni ya mtihani wa darasa la nane mwaka jana.
Akihutubu katika eneo hilo la Borabu siku ya Jumapili, mwanasiasa Nyandoro Kambi alisema kuwa kutokana na matokeo duni ya mtihani wa darasa la nane mwaka jana, walimu wanastahili kutia juhudi kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa.
Kambi alisema kuwa hali hiyo haingekuwepo iwapo karatasi na vitabu vya marudio vilivyo pokezwa shule mbalimbali kupitia kwa wakfu wake vingetumika vizuri kwa manufaa ya wanafunzi.
"Kwa kweli mwaka jana shule mbalimbali za msingi za umma zilipokezwa vitabu na karatasi za marudio kupitia kwa wakfu wangu na hata pia wahisani, ila hatuwezi tukaona la kufurahisha hata baada ya shule hizo kupokezwa vitabu hivyo,” alisema Kambi.
Aliongeza, “Sasa wakati umefika kwa walimu wa shule husika kutia bidii kuhakikisha kuwa hali hiyo haishuhudiwi tena."
Kambi alisema kuwa tume ya uajiri wa walimu TSC inastahili kuwapa uhamisho baadhi ya walimu wakuu wa shule ambao wamekuwa wakihudumu katika shule mbalimbali kwa muda mrefu, akihoji kuwa shule nyingi katika eneo hilo zina walimu wakutosha na haifai matokeo kuwa duni.
"Wakati umefika kwa tume ya TSC kuanza kuwapa uhamisho walimu ambao wamekuwa wakihudumu katika shule mbalimbali kwa muda mrefu. Hali hii huenda ikawa chanzo cha shule za sehemu hii kuwa na matokeo duni kwa maana ni jambo lakushangaza kuwa shule nyingi zilikuwa na alama za mkato kati ya 150- 240," alisema Kambi.