Mwakilishi wa wadi ya Bosamaro kaunti ya Nyamira Boniface Ombori amesema hatakubali kuona millioni 21 za wananchi zikitumika vibaya katika ujenzi wa soko la Mosobeti.
Kulingana na mwakilishi huyo ujenzi wa soko hilo ambao tayari umeanzishwa si ujenzi wa kisasa jinsi ilivyopendekezwa na wabunge wa kaunti hiyo huku akisema wananchi hawakuhusishwa kutoa maoni yao kabla ujenzi huo kuanza.
Ombori alisema tayari ameandikia bunge la kaunti hiyo barua ili kusimamisha ujenzi huo.
“Nimeandikia bunge la kaunti barua ili ujenzi huu usimamishwe hadi wananchi watoe maoni yao jinsi wangependa wajengewe soko la kisasa, kamati ya soko na mwankandarasi wajulikane ili yote yafanyika kiutaratibu,” aliongeza Ombori
Haya yanajiri baada ya wakazi wa kaunti hiyo kukataa ujenzi huo wiki jana jambo ambalo sasa limepata uungwaji mkono na mwakilishi huyo.
“Mimi kama mwakilishi wadi siwezi kunyamanza kamwe nikiona pesa za wananchi zikipotea, ujenzi wa soko la Mosobeti hauna msingi wowote wa kupendeza, hakuna ramani ya ujenzi huo, wananchi hawajahusishwa na kamati ya soko haijui chochote,” alisema Ombori.